Wednesday, April 29, 2015

MABARAZA YA WAFANYAKAZI, TAASISI ZA ELIMU YA JUU WATAKIWA KUFANYA KAZI WA WELEDI

 Naibu Waziri wa Fedha (Sera) Mhe. Mwigulu Nchemba wakati akizindua Baraza la Pili la Wafanyakazi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) leo mjini Bagamoyo.
Wajumbe wa Baraza la Pili la Wafanyakazi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) wakiimba wimbo wa mshikamano daima kabla ya kuanza kwa mkutano wao leo mjini Bagamoyo.
 Wajumbe na viongozi wa Baraza la Pili la Wafanyakazi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) wakiwa katika picha ya pamoja na Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Mwigulu Nchemba (katikati) mara baada ya kuzinduliwa kwa baraza hilo leo mjini Bagamoyo. Picha na Aron Msigwa/MAELEZO.
**********************************
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
SERIKALI imeyata Mabaraza ya wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya juu kote nchini kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia weledi, kanuni na sheria zinazosimamia  mabaraza hayo ili yawe chachu katika kuleta maendeleo ya Elimu  na mabadiliko ya kiuchumi ya taasisi hizo.
Kauli hiyo imetolewa  na Naibu Waziri wa Fedha (Sera) Mhe. Mwigulu Nchemba wakati akizindua Baraza la Pili la Wafanyakazi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) lililojumuisha wawakilishi kutoka matawi 6 ya taasisi hiyo  katika mikoa ya Kigoma, Singida, Mwanza , Mtwara, Dar es salaam na Mbeya.
Mhe. Mwigulu amesema kuwa iwapo mabaraza hayo yatazingatia weledi katika kusimamia masuala mbalimbali ya taasisi hizo nchini  yataleta mabadiliko ya kiutendaji katika usimamizi wa mapato na matumizi  na kutoa  ushauri utakaoisaidia Serikali kutekeleza mipango mbalimbali ya  maendeleo.
Mhe. Mwigulu ameeleza  kuwa endapo mabaraza hayo yataacha kufanya kazi kwa mazoea na kujikita katika kuzingatia kanuni na taratibu zilizowekwa, taasisi hizo zitaongeza uzalishaji, zitakuza mapato na kutatua kero mbalimbali za wafanyakazi mahali pa kazi.
“ Napenda niweke wazi kuwa mabaraza haya  ni muhimu sana kwa wafanyakazi, hayana tofauti na bunge ,kazi yake  kubwa ni kusimamia mapato na matumizi, kushauri taasisi na Serikali juu ya utekelezaji wa  mipango mbalimbali ikiwemo ajira kwa watumishi wapya” Amesisitiza.
Akizungumzia changamato ya uhaba wa walimu na watumishi wa kada mbalimbali  katika taasisi hiyo na taasisi nyingine za Umma za Elimu ya juu amesema Serikali inaendelea  kutenga fedha katika bajeti ya kila mwaka ili kuondoa tatizo hilo.
Aidha, amesema Serikali inaendelea kulishughulikia suala la usimamizi wa ziada ya mapato yanayozalishwa na taasisi za umma ili yaweze kupelekwa  katika maeneo mengine yenye uhitaji.
“Serikali tunaendelea kuangalia utaratibu wa kutumia ziada ya mapato inayozalishwa na taasisi mbalimbali za umma ili iweze kupelekwa katika maeneo mengine yenye uhitaji maana fedha hizi ni za umma,taasisi moja ya Serikali haiwezi kung’ania ziada ya mapato iliyozalisha, hizo ni fedha za umma lazima zikafanye kazi maeneo mengine yenye uhitaji hasa kwenye kugharamia mahitaji ya wodi za akina mama kote nchini”
Pia amesisitiza mkakati wa Serikali wa kuzifanya taasisi hizo za elimu ya juu kuwa na mamlaka yake katika kuajili watumishi wake na kjitegemea.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye ndiye Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania Dkt. Joseph Kihanda  akizungumza na wajumbe wa baraza hilo amesema kuwa taasisi hiyo katika kipindi cha miaka 5 imepata mafanikio makubwa ya kuongeza  ukusanyaji wa mapato kutoka shilingi Bilioni 6 za mwaka 2010 hadi kufikia shilingi Bilioni 18 mwaka 2014/2015.
Amesema Taasisi hiyo licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya uhaba wa miundombinu, ufinyu wa bajeti , uhaba wa walimu wenye shahada za uzamivu (PhD)  na watumishi kimeendelea kupata idadi kubwa ya wanafunzi wanaodahiliwa kutoka  7635 waliodahiliwa mwaka 2011/2012 hadi kufikia 14974 mwaka 2014/2015.
“Licha ya kuendelea kufanya vizuri taasisi yetu inakabiliwa na tatizo la waalimu katika matawi yetu yaliyo mikoani ,jambo hili hutufanya tutumie gharama kubwa kuwasafirisha kutoka makao makuu kwenda kufundisha wanafunzi wetu wanaochukua michepuo ya Biashara, Uhasibu, Rasilimali Watu, Ununuzi na Ugavi,Uhasibu katika Sekta ya Umma na Masoko na Mahusiano kwenye matawi yetu” Amesisitiza.  

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya ushauri ya wizara ya Fedha wa Taasisi hiyo Prof. Isaya Jairo akizungumza na wajumbe waliohudhuria mkutano huo amesema kuwa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA)katika kukuza na kuongeza mapato ya ndani na kupunguza utegemezi kutoka serikalini itaendelea kufanya shughuli kibiashara ,kufanya utafiti, kutoa ushauri katika Nyanja za uhasibu, ununuzi na ugavi kote nchini.

WIKI YA ELIMU, NA UZINDUZI WA TUZO YA TAALUMA YA MKUU WA MKOA IRINGA

Kauli Mbiu: NJOMBE Na 1 INAWEZEKANA.
‘’Elimu Bora ni Haki ya kila Mtoto kwa Maendeleo ya Taifa. Njombe Kuwa Na.  1. Inawezekana.’’ Hiyo ilikuwa ni Kauli Mbiu iliyopamba Kilele cha maadhimisho ya wiki ya Elimu Kimkoa katika Mkoa wa Njombe siku ya tarehe 27/04/2015; Maadhimisho hayo yaliambatana na Uzinduzi wa Tuzo ya Taaluma ya Mkuu wa Mkoa, ambapo Mkuu wa Mkoa wa Njombe Dkt. Rehema Nchimbi alikuwa Mgeni rasmi katika Maadhimisho hayo yaliyofanyika katika viwanja vya Turbo ndani ya Halmashauri ya Mji Njombe.
‘’Tuzo hiyo ina  dhamira ya kuufanya Mkoa wa Njombe kuongoza Kitaaluma kwani haki tunayo,uwezo tunao na wajibu tunao’’ Alisema Mkuu wa Mkoa wa Njombe Dkt. Rehema Nchimbi.
Tuzo hizo ziliambatana na ugawaji wa zawadi mbalimbali kwa Shule zenye ufaulu wa juu,Shule zilizoongeza ufaulu,Wanafunzi waliofanya vizuri katika mitihani ya Sekondari na Waalimu wenye ufaulu wa juu kwenye masomo wanayofundisha.
Dkt Nchimbi pia amewakaribisha wadau mbalimbali wa Elimu,Makampuni na Taasisi Mbalimbali  kujitokeza katika kuzienzi na kutoa Tuzo hizo huku zikibeba majina ya Taasisi zao.
Maadhimisho hayo pia yalipambwa na shughuli mbalimbali ikiwemo kutembelea mabanda ya shule  nakuona shughuli zinazofanywa na wanafunzi na ugawaji wa zawadi kwa waendesha pikipiki bora kwa Mkoa wa Njombe.

Imetolewa na Afisa Habari
H/Mji Njombe.
Picha ya pamoja.

Friday, April 17, 2015

BAADA YA AJALI YA JANA MTO WAMI, LEO NI HUKO KIWILA MKOANI MBEYA, HICE YAUA WATU KADHAA

Habari zilizotufikia Mtandao huu hivi punde zinasema kuwa ajali nyingine mbaya imetokea huko Kiwila maeneo ya Uwanja wa Ndege Wilaya ya Rungwe, Mkoani Mbeya, baada ya Hice iliyokuwa imebeba abiria kutumbukia mtoni na kudaiwa kuuwa watu ambao idadi yake amili kbado haijapatikana.

Aidha imeelezwa kuwa katika ajali hiyo mpaka sasa ni watu wawili akiwemo Kondakta wa Hice hiyo waliookolewa huku ikielezwa kuwa hadi sasa tayari jumla ya miili 22, imeshaopolewa kutoka kwenye Mto huo. 

Chanzo cha ajali hiyo bado hakijaweza kufahamika, lakini pia ikielezwa kuwa Hice za jijini Mbeya leo zilianza kutoa huduma ya usafiri baada ya Daladala nyingi aina ya Coaster kugoma kutoa huduma hiyo leo.
Hice hiyo inavyoonekana ikiwa mtoni baada ya kuanguka huku raia wakiishangaa.
Eneo la ajali hiyo katika daraja hili ambapo iliacha njia na kutumbukia 
Wananchi waliofika kutoa msaada wakiopoa miili na kuihifadhi eneo hili.
Mpaka sasa Miili iliyokwishaopolewa ni 22.
Gari la Polisi likiwa eneo la tukio kubeba miili. Picha kwa Hisani ya Mdau aliyeko Mbeya

VIJANA WA CCM IRINGA WAMPA NGUVU KATIBU WA MKOA HASSAN MTENGA KUKOMBOA JIMBO, LA IRINGA MJINI

Mtenga katika kikao na baadhi ya vijana hao



KIU ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Manispaa ya Iringa kukomboa jimbo la Iringa Mjini katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu inazidi kuongezeka, baada ya umoja wake wa vijana (UVCCM Manispaa ya Iringa) kuahidi kuongeza nguvu ili kuufanikisha mkakati huo.
CCM ililipoteza jimbo hilo katika Uchaguzi Mkuu wa 2010 kwa Mchungaji Msigwa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anayekaribia kumaliza muda wake.
Katika kikao kilichozikutanisha sekretarieti za umoja huo kutoka katika kata zote 18 za manispaa ya Iringa, Mwenyekiti wa UVCCM wa manispaa hiyo, Kaunda Mwaipyana alisema; “katika kukisaidia chama kushinda uchaguzi huo, kauli mbiu yetu ni chama kwanza mtu baadaye.”
“Tutapita katika matawi na kata zetu zote, tutafanya vikao, mikutano ya hadhara na kuwakumbusha vijana wajibu wa kukipigania chama chao ili mkakati wa kulikomboa jimbo ufanikiwe,” alisema.
Katibu wa CCM wa Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga aliwaongezea hamasa vijana hao kwa kuwapa seti 60 za jezi na mipira watakazozitumia kuwahamasisha vijana hao kupitia mchezo wa soka.
“CCM ina vijana wengi sana katika jimbo hili, mnahitaji kukutana na kujipanga, tumieni mbinu zote za kukutana, iwe  vikao, mikutano na hata michezo na ndio maana nimewapa msaada huu,” alisema.
Aliwataka vijana wa chama hicho kujitokeza kwenye vikao visivyo rasmi vya maeneo yao wanayoishi na kuitetea CCM kwasababu majibu ya hoja nyingi za wapinzani wanayo.
Akiwakabidhi jezi hizo, Mwenyekiti wa Umoja wa Wazazi wa CCM Mkoa wa Iringa, Ephraim Mhekwa alisema  CCM inayo nafasi ya kulikomboa jimbo hilo kama itajipanga vizuri.
“Pamoja na kwamba wapinzani walipata viti 65 katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka jana, wasisahau kwamba CCM ilipata viti 126; hesabu hiyo inadhihirisha chama chetu kinaungwa mkono mara mbili yao,” alisema.
Aliwataka vijana hao kuweka bendera za chama hicho kila panapostahili katika mitaa yote na akawasihi wasikubali kutumika na kukigawa chama kwa maslai ya wachache.
Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Mahamudu Madenge alisema CCM itaendelea kuwepo hata kama watu wasiotaka kufuata utaratibu wataondoka.
“Wameondoka wengi, wengine hii leo ni viongozi wa vyama vikubwa vya siasa. Pamoja na kuondoka kwao CCM ipo pale pale na inaendelea kupata wanachama,” alisema

Thursday, April 16, 2015

HABARI KUTOKA TFF

KILA LA KHERI YANGA JUMAMOSI
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF, Jamal Malinzi ameitakia kila la kheri timu ya Young Africans katika mchezo wake wa kesho jumamosi wa Kombe la Shirikisho barani Afrika (CC) dhidi ya timu ya Etoile du Sahel kutoka Tunisia, mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar  es salaam.

Katika salamu zake kwa klabu ya Young Africans, Rais Malinzi amewaambia wanapaswa kupambana na kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo huo wa jumamosi, ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele katika mchezo wa marudiano kwani ndio pekee kwa sasa wanaoipeperusha bendera ya Tanzania katika michuano ya kimataifa.

Young Africans imeingia katika hatua ya 16 bora Kombe l Shirikisho barani Afrika,baada ya kuzitoa BDF XI ya Botswana katika hatua ya awali kwa jumla ya mabao (3-2), kisha kuwaondoa FC Platinum ya Zimbabwe katika hatua ya kwanza kwa jumla ya mabao (5-2).

Endapo timu ya Young Africans itafanikiwa kuwaondoa Etoile du Sahel itasuburia kucheza  mechi ya mtoano (Play-off) dhidi ya timu mojawapo zitakaotolewa katika 16 bora ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika (CL).

Wakati huo huo wapinzani wa Young Africans timu ya Etoile du Sahel wanatarajiwa kuwasili  saa 9 usiku kuamkia ijumaa kwa usafiri wa Ndege ya kukodi ya kampuni ya Nouvelair   bj 4870 wakiwa na msafara wa watu 56.

Makamu wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Tunisia  (FTF), Bw. Krifa Jalel ndiye mkuu wa msafara huo akiwa na Rais wa klabu ya Etoile du Sahel (ESS) Bw.Charefeddine Ridha, wachezaji 19, benchi la ufundi lenye watu 13, waandishi wa habari 12 na wanachama 10.
Timu ya Etoile du Sahel itafikia katika hoteli ya Ledger Plaza zamani Bahari Beach eneo la Kunduchi, na kesho jioni ijumaa wanatarajiwa kufanya mazoezi katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Waamuzi wa mchezo huo ni Samwel Chirindiza, Arsenio Marenguka, Celio de Jesus Musabe, Jose Maria Bachide wote kutoka nchini Msumbuji na wanatarajiwa kuwasili leo mchana, huku kamisaa wa mchezo huo Salah Ahmed Mohamed kutokea nchini Sudan akitarajiwa kuwasili leo jioni na wote watafikia katika hoteli ya Protea iliyopo Oysterbay.

*TFF YATUMA SALAMU ZA RAMBI RAMBI KWA KHAMIS MCHA
Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF limetuma salamu za rambirambi kwa mchezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Khamis Mcha kwa kufiwa na baba yake mzazi Mcha Khamis.

TFF inampa pole Khamis pamoja na familia yake, ndugu,jamaa, marafiki na klabu ya Azam FC na kusema iko pamoja nao katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo, marehem Mcha alifariki dunia juzi kisiwani Zanzibar.

*VPL KUENDELEA LEO
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania inatarajiwa kuendelea leo ijumaa kwa mchezo mmoja, wenyeji timu ya Stand United watawakaribisha maafande wa JKT Ruvu katika uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Ligi hiyo ya Vodacom itaendelea kutimua vumbi kesho jumamosi  kwa michezo mitatu, mjini Morogoro wenyeji Polisi Morogoro watawakaribisha Ndanda FC kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Jijini Mbeya wenyeji timu ya Mbeya City watawakaribisha timu ya Simba SC kwenye uwanja wa Sokoine , huku Azam FC wakiwakaribisha wakata miwa wa Kagera Sugar kwenye uwanja wa Chamanzi Complex.

Jumapili Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania itaendelea  kwa maafande wa timu ya Ruvu Shooting  kuwakaribisha maafande wenzao wa Mgambo Shooting katika uwanja wa Mabatini - Mlandizi, huku jijini Mbeya wenyeji timu ya Prisons FC wakiwakaribisha wakata miwa wa Mtibwa Sugar.

DRFA YAIPA MBINU YANGA KUINYOA ETOILE DU SAHEL

Kuelekea mchezo wa michuano ya kombe la shirikisho barani afrika kati ya Yanga dhidi ya Etoile Du Sahel ya Tunisia utakaopigwa jumamosi hii April 18 katika uwanja wa taifa,Chama cha soka mkoa wa Dar es salaam DRFA,kimeitabiria makubwa klabu hiyo ya Jangwani kuvuka katika kizingiti hicho kigumu kwa mchezo wa nyumbani na ugenini dhidi ya wababe hao wa Tunisia.
Mwenyekiti wa chama hicho Almasi Kasongo,amesema ili yanga ifanye vizuri katika mechi hiyo na kuwapa raha mashabiki wake na watanzania kwa ujumla,ni lazima icheze kwa uangalifu mkubwa na kukwepa kuendana na style ya kupoozesha mpira wanayoitumia wapinzani katika mechi za ugenini.
kasongo amelishauri benchi la ufundi la Yanga chini ya makocha Hans Pluijm na msaidizi wake Charles Mkwasa,kutumia mbinu ya kushambulia kwa muda wote ili kuwaduwaza wapinzani ambao wakati mwingine hutumia mbinu ya kufanya mashambulizi ya kushtukiza.
Ametoa wito pia kwa mashabiki wa soka mkoa wa Dar es salaam na maeneo ya jirani, kujitokeza kwa wingi siku ya jumamosi kuishangilia Yanga ambao wanaliwakilisha taifa katika mashindano hayo ya vilabu barani afrika.
Hata hivyo DRFA inaamini kuwa Yanga ambayo ni moja ya timu zake zilizopo katika mkoa wa Dar es salaam haina sababu ya kutofanya vizuri katika mchezo huo, kutokana na kuwa na kikosi kizuri kilichovisambaratisha katika michuano hiyo vilabu vya BDF ya Botswana pamoja na Platinum ya Zimbabwe.

SHEREHE ZA MAADHIMISHO YA KILELE CHA SIKU YA ELIMU NA MAZINGIRA KWA SHULE ZA SEKONDARI NA MSINGI MANISPAA YA ILALA

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Maktaba wakicheza ngoma wakati wa sherehe za Maazimisho ya Kilele cha Siku ya Elimu Wilaya ya Ilala na Kilele cha Maadhimisho ya Mazingira kwa Shule za Msingi na Sekondari za Manispaa ya Ilala 'Mazingira Bora Kwa Elimu  Bora'.
 Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Diamond,  Hashimu Semvua, akikabidhiwa Tuzo ya kwanza ya Mazingira ya Kata ya Gerezani  Manispaa ya Ilala, na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi.
 Mkuu wa Wilaya Ilala, Raymond Mushi, akifunga rasmi Siku ya Elimu na Kilele cha Maazimisho ya Mazingira Shule za  Msingi na Sekondari Manispaa ya Ilala.
 Mgeni rasmi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi,  akisikiliza maelezo kutoka kwa mwanafunzi Fatuma Omari mwanafunzi wa kidatu cha pili  shule ya Sekondari  Benjameni Mkapa, wakati alipokuwa akitembelea maonyesho ya Sayansi ya wanafunzi hao katika sherehe hizo za kilele cha Siku ya Elimu Wilaya ya Ilala. Aliyeshika Maiki ni Mwalimu Elizabeth Mapela wa elimu maalum.
Mkurungezi wa Manispaa ya Ilala Isaya Mwangurume, akimkaribisha mgeni rasmi (kushoto kwake) Kulia ni Mwenyekiti wa Uchumi na Hunduma za Jamii Manispaa ya Ilala, Angel Malembeka. 
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Diamond,  Hashimu Semvua, akipongezwa na walimu wenzake baada ya kupokea Tuzo ya kwanza ya Mazingira ya Kata ya Gerezani  Manispaa ya Ilala. Picha na Miraii Msala

Balozi wa Uingereza Nchini Tanzania akutana na Waziri wa Ardhi

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa William Lukuvi akizungumza na Balozi wa Uingereza hapa nchini Bi. Dianna Melrose wakati balozi huyo alipomtembelea Mheshimiwa Lukuvi ofisini kwake kujadiliana masuala mbalimbali yanayohusu uendelezaji wa  uendelezaji wa sekta ya ardhi nchini Tanzania.
Picha/ Nanyaro,Clarence - Wizara ya Ardhi.

MIMI SIJAFA NI UZUSHI WA WAJINGA WA MITANDAO TU: HUSSEIN MACHOZI

Habari zilizoenea katika mitandao ya kijamii kuhusu Mwanamuziki wa kizazi kipya nchini Hussein Machozi, zikimzushia kifo si za kweli na ni jambo ambalo linatakiwa kukemewa kwa nguvu zote kwani ni upotoshaji wa habari.

Akizungumza na mtandao huu kwa njia ya Simu muda mchache uliopita Machozi alisema kuwa amesikitishwa na uzushi huo ulioenezwa kwenye mitandao ya Kijamii, na kuwaondoa hofu Ndugu, Jamaa, Marafiki na Mashabiki wake kuwa yupo fiti.

''Mimi nipo fiti na naendelea na majukumu yangu ya kila siku kama kawaida, hizo ni habari za uzushi tu ambazo sielewi lengo lake ni nini, labda ndo kunitakiwa maisha marefu lakini si jambo zuri na hata huyo alieanzisha na kusambaza kwenye mitandao alikuwa na lengo lake ambalo mimi na hata wewe mwandishi hatulijui, 

Hivyo kwa kuwa ameshakamilisha dhamira yake na wengi wameshitushwa na habari hii, basi nadhani ameshatimiza alilokuwa amekusudia, hivyo tumuachia Mwenyezi Mungu tu''. alisema Machozi

Habari za uzushi kama hizi zimekuwa zikienea kwa kasi katika mitandao ya Kijamii, ambapo siku za hivi karibuni pia ilisambazwa habari katika mitandao kuwa aliyekuwa Kocha wa Simba, Mzee Kibaden amefariki, jambo ambalo halikuwa la kweli, hivyo wanajamii tuungane na hasa watumiaji wa mitandao kukemea watu hawa wasiouwa maana halisi  na matumizi ya mitandao ya kijamii.

TUKIUNGANA TUNAWEZA KUWAKOMESHA

MASHABIKI WA SIMBA KUISHANGILIA YANGA

Katika kile kinachotarajiwa na mashabiki wengi wa soka la Bongo ni tukio la mashabiki wa timu Kongwe za nchini Yanga na Simba, siku watakapoingia uwanjani kwa lengo la kuishangilia timu pinzani wakatiikicheza.

Kutokana na Ligi Kuu ya Tanzania bara kuwa ngumu msimu huu, huku timu za Yanga na Mabingwa watetezi Azam Fc wakifukuzana katika mbio hizo za kuwania ubingwa na kutofautiana kwa Pointi saba na Simba nao wakikesha huku wakiiombea mabaya Azam na wakijitahidi angalau kumaliza Ligi wakiwa nafasi ya pili, hii ndiyo hasa sababu kubwa itakayowabadilisha mashabiki wa timu hizi kushangilia wapinzani wa jadi.

Yanga inaongoza Ligi hiyo ikiwa na jumla ya Pointi 46, baada ya kucheza mechi 21, wakifuatiwa na Azam Fc wenye Pointi 39,nao pia wakicheza mechi 21 huku Simba wakiwapumulia Azam Fc wakiwa na Pointi 35 nao pia wakicheza mechi 21 na Kagera Sugar wakifuatia wakiwa na Pointi 31 wakicheza mechi 22.

Kwa matokeo hayo Mabinwa watetezi Azam Fc bado wana mechi ngumu mkononi ambazo ni kati yao na Yanga na Simba, ambapo mechi hizi hsa ndizo zitawasilimisha mashabiki wa timu za jadi watakaolazimika kushangilia timu pinzani.

Siku ya mechi ya Yanga na Azam Fc, mashabiki wa Simba watalazimika kuishangilia Yanga ili Yanga ishinde na Azam Fc wapoteze mchezo ili Simba iendelee kuwa na uhakika wa kuipata nafasi ya pili ili iweze kushiriki michuano ya Kimataifa.

Na siku ya mechi ya Simba na Azam Fc, mashabiki wa Yanga nao watalazimika kuishangilia Simba, ili Azam Fc waendelee kuchechemea katika mbio hizo za kuwania ubingwa

IMETOSHA YAWASILI MWANZA,

Kutoka (kushoto) Wakuvwanga, Zaytuni Biboze, Salome Gregory, Henry Mdimu na  msanii wa muziki wa reggae Jhikoman Manyika wakiwa nje ya uwanja wa ndege jijini Mwanza mara baada ya kuwasili leo asubuhi.
Ujumbe wa taasisi ya Imetosha inayojishughulisha na utoaji elimu juu ya kumaliza unyanyapaa,  ukatili na mauaji kwa watu wenye ualbino nchini uliwasili jijini Mwanza leo hii saa 2 asubuhi kwa ziara ya siku 3 ambapo kati siku hizo tatu ujumbe huo utakutana na viongozi wa ki serikali na usalama wa baadhi ya mikoa na wilaya za kanda ya ziwa ikiwemo Mwanza na Shinyanga. Lengo la mikutano hiyo ni kamati kujitambulisha kwa viongozi hao na kuwaeleza nini Imetosha inatarajia kufanya katika kanda hii mwezi ujao ambako pamekuwa na matukio mengi ya ukatili na mauaji kwa watu wenye ualbino nchini Tanzania. 

 Vile vile kamati itakuwa na siku moja ambapo itatembelea vyombo ya habari vya jijini hapa kabla ya kurejea Dar es Salaam.

Habari na picha na Mkala Fundikira wa Mkalamatukio/keronyingi blog

LIBENEKE JIPYA MTANDAONI

Untitled-1 copy
KWA MATUKIO MBALIMBALI YANAYOHUSU MASUALA YA SIASA ZIKIWEMO HABARI MAKALA FUPIFUPI , VITUKO , KUJIFAGILIA NA UWAJIBIKAJI WA WANASIASA KWA JAMII TEMBELEA www.politikstz.blogspot.com ILI UPATE KUJUA, KUELIMIKA NA KUBURUDIKA. PIA UNAWEZA KUTUTUMIA HABARI, MATUKIO YA PICHA NA MAKALA FUPIFUPI LAKINI ZISIWE HABARI ZA KUCHAFUA HALI YA HEWA AMA KUMCHAFUA MTU TUTUMIE KWA EMAIL HII www.politikstz@gmail.comTUTASHUKURU KWA USHIRIKIANO WENU.