Thursday, April 16, 2015

HABARI KUTOKA TFF

KILA LA KHERI YANGA JUMAMOSI
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF, Jamal Malinzi ameitakia kila la kheri timu ya Young Africans katika mchezo wake wa kesho jumamosi wa Kombe la Shirikisho barani Afrika (CC) dhidi ya timu ya Etoile du Sahel kutoka Tunisia, mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar  es salaam.

Katika salamu zake kwa klabu ya Young Africans, Rais Malinzi amewaambia wanapaswa kupambana na kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo huo wa jumamosi, ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele katika mchezo wa marudiano kwani ndio pekee kwa sasa wanaoipeperusha bendera ya Tanzania katika michuano ya kimataifa.

Young Africans imeingia katika hatua ya 16 bora Kombe l Shirikisho barani Afrika,baada ya kuzitoa BDF XI ya Botswana katika hatua ya awali kwa jumla ya mabao (3-2), kisha kuwaondoa FC Platinum ya Zimbabwe katika hatua ya kwanza kwa jumla ya mabao (5-2).

Endapo timu ya Young Africans itafanikiwa kuwaondoa Etoile du Sahel itasuburia kucheza  mechi ya mtoano (Play-off) dhidi ya timu mojawapo zitakaotolewa katika 16 bora ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika (CL).

Wakati huo huo wapinzani wa Young Africans timu ya Etoile du Sahel wanatarajiwa kuwasili  saa 9 usiku kuamkia ijumaa kwa usafiri wa Ndege ya kukodi ya kampuni ya Nouvelair   bj 4870 wakiwa na msafara wa watu 56.

Makamu wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Tunisia  (FTF), Bw. Krifa Jalel ndiye mkuu wa msafara huo akiwa na Rais wa klabu ya Etoile du Sahel (ESS) Bw.Charefeddine Ridha, wachezaji 19, benchi la ufundi lenye watu 13, waandishi wa habari 12 na wanachama 10.
Timu ya Etoile du Sahel itafikia katika hoteli ya Ledger Plaza zamani Bahari Beach eneo la Kunduchi, na kesho jioni ijumaa wanatarajiwa kufanya mazoezi katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Waamuzi wa mchezo huo ni Samwel Chirindiza, Arsenio Marenguka, Celio de Jesus Musabe, Jose Maria Bachide wote kutoka nchini Msumbuji na wanatarajiwa kuwasili leo mchana, huku kamisaa wa mchezo huo Salah Ahmed Mohamed kutokea nchini Sudan akitarajiwa kuwasili leo jioni na wote watafikia katika hoteli ya Protea iliyopo Oysterbay.

*TFF YATUMA SALAMU ZA RAMBI RAMBI KWA KHAMIS MCHA
Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF limetuma salamu za rambirambi kwa mchezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Khamis Mcha kwa kufiwa na baba yake mzazi Mcha Khamis.

TFF inampa pole Khamis pamoja na familia yake, ndugu,jamaa, marafiki na klabu ya Azam FC na kusema iko pamoja nao katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo, marehem Mcha alifariki dunia juzi kisiwani Zanzibar.

*VPL KUENDELEA LEO
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania inatarajiwa kuendelea leo ijumaa kwa mchezo mmoja, wenyeji timu ya Stand United watawakaribisha maafande wa JKT Ruvu katika uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Ligi hiyo ya Vodacom itaendelea kutimua vumbi kesho jumamosi  kwa michezo mitatu, mjini Morogoro wenyeji Polisi Morogoro watawakaribisha Ndanda FC kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Jijini Mbeya wenyeji timu ya Mbeya City watawakaribisha timu ya Simba SC kwenye uwanja wa Sokoine , huku Azam FC wakiwakaribisha wakata miwa wa Kagera Sugar kwenye uwanja wa Chamanzi Complex.

Jumapili Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania itaendelea  kwa maafande wa timu ya Ruvu Shooting  kuwakaribisha maafande wenzao wa Mgambo Shooting katika uwanja wa Mabatini - Mlandizi, huku jijini Mbeya wenyeji timu ya Prisons FC wakiwakaribisha wakata miwa wa Mtibwa Sugar.

DRFA YAIPA MBINU YANGA KUINYOA ETOILE DU SAHEL

Kuelekea mchezo wa michuano ya kombe la shirikisho barani afrika kati ya Yanga dhidi ya Etoile Du Sahel ya Tunisia utakaopigwa jumamosi hii April 18 katika uwanja wa taifa,Chama cha soka mkoa wa Dar es salaam DRFA,kimeitabiria makubwa klabu hiyo ya Jangwani kuvuka katika kizingiti hicho kigumu kwa mchezo wa nyumbani na ugenini dhidi ya wababe hao wa Tunisia.
Mwenyekiti wa chama hicho Almasi Kasongo,amesema ili yanga ifanye vizuri katika mechi hiyo na kuwapa raha mashabiki wake na watanzania kwa ujumla,ni lazima icheze kwa uangalifu mkubwa na kukwepa kuendana na style ya kupoozesha mpira wanayoitumia wapinzani katika mechi za ugenini.
kasongo amelishauri benchi la ufundi la Yanga chini ya makocha Hans Pluijm na msaidizi wake Charles Mkwasa,kutumia mbinu ya kushambulia kwa muda wote ili kuwaduwaza wapinzani ambao wakati mwingine hutumia mbinu ya kufanya mashambulizi ya kushtukiza.
Ametoa wito pia kwa mashabiki wa soka mkoa wa Dar es salaam na maeneo ya jirani, kujitokeza kwa wingi siku ya jumamosi kuishangilia Yanga ambao wanaliwakilisha taifa katika mashindano hayo ya vilabu barani afrika.
Hata hivyo DRFA inaamini kuwa Yanga ambayo ni moja ya timu zake zilizopo katika mkoa wa Dar es salaam haina sababu ya kutofanya vizuri katika mchezo huo, kutokana na kuwa na kikosi kizuri kilichovisambaratisha katika michuano hiyo vilabu vya BDF ya Botswana pamoja na Platinum ya Zimbabwe.

SHEREHE ZA MAADHIMISHO YA KILELE CHA SIKU YA ELIMU NA MAZINGIRA KWA SHULE ZA SEKONDARI NA MSINGI MANISPAA YA ILALA

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Maktaba wakicheza ngoma wakati wa sherehe za Maazimisho ya Kilele cha Siku ya Elimu Wilaya ya Ilala na Kilele cha Maadhimisho ya Mazingira kwa Shule za Msingi na Sekondari za Manispaa ya Ilala 'Mazingira Bora Kwa Elimu  Bora'.
 Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Diamond,  Hashimu Semvua, akikabidhiwa Tuzo ya kwanza ya Mazingira ya Kata ya Gerezani  Manispaa ya Ilala, na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi.
 Mkuu wa Wilaya Ilala, Raymond Mushi, akifunga rasmi Siku ya Elimu na Kilele cha Maazimisho ya Mazingira Shule za  Msingi na Sekondari Manispaa ya Ilala.
 Mgeni rasmi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi,  akisikiliza maelezo kutoka kwa mwanafunzi Fatuma Omari mwanafunzi wa kidatu cha pili  shule ya Sekondari  Benjameni Mkapa, wakati alipokuwa akitembelea maonyesho ya Sayansi ya wanafunzi hao katika sherehe hizo za kilele cha Siku ya Elimu Wilaya ya Ilala. Aliyeshika Maiki ni Mwalimu Elizabeth Mapela wa elimu maalum.
Mkurungezi wa Manispaa ya Ilala Isaya Mwangurume, akimkaribisha mgeni rasmi (kushoto kwake) Kulia ni Mwenyekiti wa Uchumi na Hunduma za Jamii Manispaa ya Ilala, Angel Malembeka. 
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Diamond,  Hashimu Semvua, akipongezwa na walimu wenzake baada ya kupokea Tuzo ya kwanza ya Mazingira ya Kata ya Gerezani  Manispaa ya Ilala. Picha na Miraii Msala

Balozi wa Uingereza Nchini Tanzania akutana na Waziri wa Ardhi

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa William Lukuvi akizungumza na Balozi wa Uingereza hapa nchini Bi. Dianna Melrose wakati balozi huyo alipomtembelea Mheshimiwa Lukuvi ofisini kwake kujadiliana masuala mbalimbali yanayohusu uendelezaji wa  uendelezaji wa sekta ya ardhi nchini Tanzania.
Picha/ Nanyaro,Clarence - Wizara ya Ardhi.

MIMI SIJAFA NI UZUSHI WA WAJINGA WA MITANDAO TU: HUSSEIN MACHOZI

Habari zilizoenea katika mitandao ya kijamii kuhusu Mwanamuziki wa kizazi kipya nchini Hussein Machozi, zikimzushia kifo si za kweli na ni jambo ambalo linatakiwa kukemewa kwa nguvu zote kwani ni upotoshaji wa habari.

Akizungumza na mtandao huu kwa njia ya Simu muda mchache uliopita Machozi alisema kuwa amesikitishwa na uzushi huo ulioenezwa kwenye mitandao ya Kijamii, na kuwaondoa hofu Ndugu, Jamaa, Marafiki na Mashabiki wake kuwa yupo fiti.

''Mimi nipo fiti na naendelea na majukumu yangu ya kila siku kama kawaida, hizo ni habari za uzushi tu ambazo sielewi lengo lake ni nini, labda ndo kunitakiwa maisha marefu lakini si jambo zuri na hata huyo alieanzisha na kusambaza kwenye mitandao alikuwa na lengo lake ambalo mimi na hata wewe mwandishi hatulijui, 

Hivyo kwa kuwa ameshakamilisha dhamira yake na wengi wameshitushwa na habari hii, basi nadhani ameshatimiza alilokuwa amekusudia, hivyo tumuachia Mwenyezi Mungu tu''. alisema Machozi

Habari za uzushi kama hizi zimekuwa zikienea kwa kasi katika mitandao ya Kijamii, ambapo siku za hivi karibuni pia ilisambazwa habari katika mitandao kuwa aliyekuwa Kocha wa Simba, Mzee Kibaden amefariki, jambo ambalo halikuwa la kweli, hivyo wanajamii tuungane na hasa watumiaji wa mitandao kukemea watu hawa wasiouwa maana halisi  na matumizi ya mitandao ya kijamii.

TUKIUNGANA TUNAWEZA KUWAKOMESHA

MASHABIKI WA SIMBA KUISHANGILIA YANGA

Katika kile kinachotarajiwa na mashabiki wengi wa soka la Bongo ni tukio la mashabiki wa timu Kongwe za nchini Yanga na Simba, siku watakapoingia uwanjani kwa lengo la kuishangilia timu pinzani wakatiikicheza.

Kutokana na Ligi Kuu ya Tanzania bara kuwa ngumu msimu huu, huku timu za Yanga na Mabingwa watetezi Azam Fc wakifukuzana katika mbio hizo za kuwania ubingwa na kutofautiana kwa Pointi saba na Simba nao wakikesha huku wakiiombea mabaya Azam na wakijitahidi angalau kumaliza Ligi wakiwa nafasi ya pili, hii ndiyo hasa sababu kubwa itakayowabadilisha mashabiki wa timu hizi kushangilia wapinzani wa jadi.

Yanga inaongoza Ligi hiyo ikiwa na jumla ya Pointi 46, baada ya kucheza mechi 21, wakifuatiwa na Azam Fc wenye Pointi 39,nao pia wakicheza mechi 21 huku Simba wakiwapumulia Azam Fc wakiwa na Pointi 35 nao pia wakicheza mechi 21 na Kagera Sugar wakifuatia wakiwa na Pointi 31 wakicheza mechi 22.

Kwa matokeo hayo Mabinwa watetezi Azam Fc bado wana mechi ngumu mkononi ambazo ni kati yao na Yanga na Simba, ambapo mechi hizi hsa ndizo zitawasilimisha mashabiki wa timu za jadi watakaolazimika kushangilia timu pinzani.

Siku ya mechi ya Yanga na Azam Fc, mashabiki wa Simba watalazimika kuishangilia Yanga ili Yanga ishinde na Azam Fc wapoteze mchezo ili Simba iendelee kuwa na uhakika wa kuipata nafasi ya pili ili iweze kushiriki michuano ya Kimataifa.

Na siku ya mechi ya Simba na Azam Fc, mashabiki wa Yanga nao watalazimika kuishangilia Simba, ili Azam Fc waendelee kuchechemea katika mbio hizo za kuwania ubingwa

IMETOSHA YAWASILI MWANZA,

Kutoka (kushoto) Wakuvwanga, Zaytuni Biboze, Salome Gregory, Henry Mdimu na  msanii wa muziki wa reggae Jhikoman Manyika wakiwa nje ya uwanja wa ndege jijini Mwanza mara baada ya kuwasili leo asubuhi.
Ujumbe wa taasisi ya Imetosha inayojishughulisha na utoaji elimu juu ya kumaliza unyanyapaa,  ukatili na mauaji kwa watu wenye ualbino nchini uliwasili jijini Mwanza leo hii saa 2 asubuhi kwa ziara ya siku 3 ambapo kati siku hizo tatu ujumbe huo utakutana na viongozi wa ki serikali na usalama wa baadhi ya mikoa na wilaya za kanda ya ziwa ikiwemo Mwanza na Shinyanga. Lengo la mikutano hiyo ni kamati kujitambulisha kwa viongozi hao na kuwaeleza nini Imetosha inatarajia kufanya katika kanda hii mwezi ujao ambako pamekuwa na matukio mengi ya ukatili na mauaji kwa watu wenye ualbino nchini Tanzania. 

 Vile vile kamati itakuwa na siku moja ambapo itatembelea vyombo ya habari vya jijini hapa kabla ya kurejea Dar es Salaam.

Habari na picha na Mkala Fundikira wa Mkalamatukio/keronyingi blog

LIBENEKE JIPYA MTANDAONI

Untitled-1 copy
KWA MATUKIO MBALIMBALI YANAYOHUSU MASUALA YA SIASA ZIKIWEMO HABARI MAKALA FUPIFUPI , VITUKO , KUJIFAGILIA NA UWAJIBIKAJI WA WANASIASA KWA JAMII TEMBELEA www.politikstz.blogspot.com ILI UPATE KUJUA, KUELIMIKA NA KUBURUDIKA. PIA UNAWEZA KUTUTUMIA HABARI, MATUKIO YA PICHA NA MAKALA FUPIFUPI LAKINI ZISIWE HABARI ZA KUCHAFUA HALI YA HEWA AMA KUMCHAFUA MTU TUTUMIE KWA EMAIL HII www.politikstz@gmail.comTUTASHUKURU KWA USHIRIKIANO WENU.